<div class="bbWrapper"></div>
- Tunachokijua
- Nanasi huhusishwa na kuharibu ujauzito mchanga kwa wanawake.
Athari hii hutokana na uwepo wa vimeng’enya vya bromelain ambavyo kiasili hupatikana kwenye nanasi pekee.
Kwa mujibu wa USDA, Bromelain ni kundi kubwa la vimeng’enya vinavyopatikana kwenye tunda la nanasi ambavyo pamoja na kazi zingine, husaidia mmeng’enyo wa vyakula vyenye asili ya protini pamoja na kutibu au kudhibiti uvimbe mwilini.
Kuhusu ujauzito, ni kweli kuwa Vidonge vyenye bromelain huwa havishauriwi kumezwa na mwanamke mjamzito kwa sababu vinaweza kumfanya apoteze damu nyingi pamoja na kuharibu ujauzito. Hii inatokana na uwepo wa dozi ya kutosha kwenye dawa hizo inayoweza kuleta athari.
Hata hivyo, JamiiForums imebaini kuwa Bromelain inayopatikana kwenye nanasi ni chache sana kuweza kuleta athari zozote kwa ujauzito, haifikii kiasi cha kawaida cha dozi ndogo inayohitajika kuamsha uchungu wa mapema.
Pia, hakuna tafiti za kisayansi zinazothibitisha madhara haya kwa binadamu.
Kwa maana hiyo, nanasi linabaki kuwa tunda bora na salama kwa mwanamke mjamzito kutokana na uwepo wa virutubisho vingi vinavyofaa kwa mama na mtoto.