KWELI Mwanamke anaweza kubeba Ujauzito wa watoto mapacha wenye baba tofauti

KWELI Mwanamke anaweza kubeba Ujauzito wa watoto mapacha wenye baba tofauti

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
<div class="bbWrapper"></div>
 
Tunachokijua
Ujauzito hutokea baada ya kuungana kwa mbegu ya kiume na yai la mwanamke, tendo ambalo kitaalam huitwa urutubishaji (Fertilization). Tendo hili hutokea kwenye siku maalum katika mzunguko wa hedhi ya mwanamke.

Baada ya kutokea kwa urutubishaji huu, yai pamoja na mwili wa mwanamke kwa ujumla hutengeneza mfumo imara usioruhusu kutokea kwa urubishwaji wa mara ya pili kwenye yai moja. Ni mwanzo wa takriban siku 280 za kulea ujauzito mpya hadi pindi ambapo muda wa kujifungua utafika.

Katika hali ya kawaida, ujauzito wa mwanamke huhusisha baba mmoja wa mtoto. Hii inatokana na ukweli kuwa wanawake wengi hutoa yai moja lililopevuka katika kila mzunguko mmoja wa hedhi.

Ujauzito wa watoto wawili wenye baba tofauti
Kwa mujibu wa Taasisi ya Afya ya Marekani (NHI), baadhi ya wanawake hutoa yai lililopevuka zaidi ya moja kwenye mzunguko mmoja wa hedhi.

Ikiwa mwanamke atashiriki tendo la ndoa na mwanaume mmoja kisha wakafanikiwa kufanya urutubishaji, baadae mwanamke huyo akashiriki tena tendo la ndoa na mwanaume mwingine baada ya kutolewa kwa yai lingine ndani ya mzunguko huo mmoja, urutubishaji mwingine wa mara ya pili unaweza kutokea.

Tendo hili huitwa Heteropaternal superfecundation, humaanisha kuwa mwanamke amepata ujauzito wa watoto wawili (mapacha), kwenye mzunguko mmoja wa hedhi uliohusisha mayai mawili, ambao baba zao ni tofauti.

Utafiti wenye kichwa cha habari "How frequent is heteropaternal superfecundation?" wa Wenk RE et al, unabainisha kuwa visa hivi huwa havitokei kwa namba kubwa. Mathalani, katika utafiti wao uliohusisha wazazi 39,000 wenye watoto mapacha wasiofanana, ni 2.4% ndio waligundulika kuwa na baba tofauti.

Hivyo, kwa kuzingatia rejea hizi muhimu, pamoja na mazungumzo tuliyofanya na madaktari bingwa wa Masuala ya uzazi, JamiiForums inakubaliana na hoja kuwa hali hii ipo, na inaweza kutokea kwa wanawake wachache sana.
Back
Top Bottom